WATUMISHI WA IRUWASA WAPATIWA MAFUNZO YA AFYA YA AKILI, UNYANYASAJI WA KIJINSIA NA MAGONJWA YASIYO YA KUAMBUKIZA
Watumishi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Iringa (IRUWASA) wamepata mafunzo kuhusu afya ya akili, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa afya ya akili na ustawi wa watumishi katika mazingira ya kazi na maisha ya kila siku.
Mafunzo haya yametolewa na Dkt. Garvin Kweka, daktari bingwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), katika ukumbi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Kituo cha Iringa.
Katika mafunzo haya, watumishi wamepata fursa ya kujifunza masuala mbalimbali yanayohusu afya ya akili, umuhimu wa kuitunza, pamoja na kuongeza uelewa kuhusu namna ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kuathiri ustawi wa mtu katika maisha na mazingira ya kazi.
Aidha, watumishi wamepata elimu kuhusu unyanyasaji wa kijinsia, ikilenga kuongeza uelewa juu ya aina mbalimbali za unyanyasaji, madhara yake na umuhimu wa kujenga mazingira salama, yenye heshima na usawa kwa wote.
Sambamba na hilo, mafunzo hayo yamejumuisha elimu kuhusu magonjwa yasiyo ya kuambukiza, kwa lengo la kuhamasisha watumishi kuzingatia afya zao kupitia uelewa wa vihatarishi, kinga na umuhimu wa kuchukua hatua za mapema katika kulinda afya zao.
Kupitia mafunzo haya, IRUWASA inaendelea kuweka msisitizo katika umuhimu wa afya na ustawi wa watumishi, kwa kutambua kuwa afya bora ni miongoni mwa mambo muhimu yanayochangia ufanisi kazini na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.