News 15th June, 2026

News Images

IRUWASA KUANZA KUTEKELEZA MRADI WA UFUNGAJI MIFUMO YA KISASA YA UTOAJI HUDUMA ZA MAJISAFI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Iringa (IRUWASA), kwa kushirikiana na kampuni ya Greentech kutoka Korea, inaendelea na zoezi la utafiti wa kina kwa ajili ya maandalizi ya utekelezaji wa mradi wa kufunga mfumo wa kisasa wa utoaji huduma za maji safi katika mji wa Iringa.

Mradi huo unatarajiwa kuanza kutekelezwa mwezi Septemba mwaka 2026 na kukamilika mwaka 2028 kwa gharama ya Dola za Kimarekani milioni 8. Utekelezaji wa mradi huu ni sehemu ya juhudi za IRUWASA za kuimarisha huduma za maji kwa kutumia teknolojia za kisasa zinazolenga kuongeza ufanisi, kupunguza hasara za maji na kuboresha usimamizi wa miundombinu ya maji.

Miongoni mwa faida kubwa za mradi huo ni kupunguza kiwango cha maji yasiyolipiwa (Non-Revenue Water) kupitia uwekaji wa mifumo ya kisasa ya kugundua na kufuatilia uvujaji wa maji katika mtandao wa usambazaji. Teknolojia hiyo itasaidia kubaini haraka maeneo yenye upotevu wa maji na hivyo kuongeza mapato pamoja na ufanisi wa utoaji huduma.

Aidha, mradi huo utasaidia kupunguza gharama za uzalishaji na uendeshaji wa huduma za maji kwa kuweka mifumo ya kisasa ya kufuatilia hali ya usalama na ubora wa maji kwa wakati halisi. Mfumo huo utawezesha wataalamu wa IRUWASA kufanya maamuzi ya haraka na sahihi kuhusu uendeshaji wa mitambo na usimamizi wa huduma.

Kukamilika kwa mradi huu wananchi wa Iringa wanatarajiwa kunufaika na huduma bora zaidi za majisafi, zenye uhakika, salama na endelevu zenye kuendana na kasi ya ukuaji wa teknolojia.


Posted On: 15th June, 2026
News Source: NLUPC Reporters