News 15th June, 2026
IRUWASA YAPEPERUSHA BENDERA YA TANZANIA KIMATAIFA
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Iringa IRUWASA imeendelea kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania baada ya kuibuka mshindi wa pili katika tuzo za “Best of the Best Performers” zilizotolewa na Eastern and Southern Africa Water and Sanitation Regulators Association mwaka 2025.
Tuzo hii ilitolewa kupitia mfumo wa kimataifa wa kulinganisha utendaji wa taasisi za maji na usafi wa mazingira kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki na Kusini (Multi-country Benchmarking), ambapo taasisi zilipimwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo utoaji wa huduma ya maji, ubora wa huduma kwa wateja, usimamizi wa fedha, ukusanyaji wa mapato pamoja na udhibiti wa upotevu wa maji.
Kutwaa nafasi hiyo kunathibitisha kuwa IRUWASA ni miongoni mwa Mamlaka bora za majisafi na usafi wa mazingira katika ukanda huu, huku ikionyesha uwezo mkubwa wa uongozi, matumizi ya teknolojia, usimamizi wa miundombinu na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Mafanikio hayo pia yanaendelea kuijengea Tanzania heshima kimataifa na kuongeza imani kwa wadau, wawekezaji na mashirika mbalimbali ya maendeleo katika sekta ya maji na usafi wa mazingira.
Posted On: 15th June, 2026
News Source: NLUPC Reporters
