News 4th March, 2026
IRUWASA Yaweka Wazi Mafanikio na Mpango Mkakati wa Miaka Mitano Ijayo
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Iringa (IRUWASA) imefanya Mkutano wa Wadau wa Maji tarehe 3 Aprili 2026 katika Ukumbi wa Siasa ni Kilimo, Manispaa ya Iringa, kwa lengo la kueleza mafanikio ya miaka mitano iliyopita pamoja na kuwasilisha mpango mkakati wa kuboresha huduma kwa miaka mitano ijayo.
Mgeni rasmi katika mkutano huo ni Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dk Linda Salekwa, akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Iringa. Akizungumza katika mkutano huo, Dk Salekwa amewasihi wananchi kuendelea kutunza vyanzo vya maji ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa rasilimali hiyo muhimu.
Aidha, aliishauri IRUWASA kuendelea kutafuta vyanzo mbadala vya maji, ikiwemo kuchakata majitaka na kuyasafisha ili yaweze kutumika tena kwa matumizi ya binadamu. Amesisitiza pia umuhimu wa mamlaka hiyo kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu matumizi sahihi ya maji na utunzaji wa mazingira ili kulinda vyanzo vya maji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa IRUWASA, Eng. David Pallangyo, Amewasilisha taarifa ya mafanikio ya mamlaka hiyo kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita. Ameleza kuwa IRUWASA imefanikiwa kufunga mita za malipo kabla zipatazo 6,500, hatua inayosaidia kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato na kudhibiti upotevu wa maji.
Eng. Pallangyo ameongeza kuwa kwa miaka mitatu mfululizo IRUWASA imekuwa Mamlaka namba moja nchini Tanzania kwa utendaji bora, na kwa kipindi cha Miaka mitano imeendelea kuwa miongoni mwa Mamlaka tatu bora zinazofanya vizuri kitaifa. Pia, mamlaka hiyo imepokea tuzo kutoka Wizara ya Maji ya Utendaji Bora wa Muda Wote (Lifetime Performance Excellence Award), ikiwa ni kutambua mchango wake katika kuboresha huduma ya maji.
Akizungumzia mipango ya Miaka mitano ijayo, Eng. Pallangyo alisema IRUWASA inatarajia kutekeleza mradi mkubwa wa uboreshaji wa huduma za majisafi kwa Manispaa ya Iringa pamoja na miji ya Ilula na Kilolo, wenye thamani ya shilingi bilioni 270. Mradi huo unalenga kuongeza upatikanaji wa maji safi, kuboresha miundombinu na kukidhi mahitaji ya wananchi yanayoongezeka.
Posted On: 4th March, 2026
News Source: NLUPC Reporters
