News 10th December, 2025

News Images

NAIBU WAZIRI WA MAJI AFANYA ZIARA YA KIKAZI MKOANI IRINGA, ASISITIZA UWAZIBIKAJI NA UBUNIFU KATIKA SEKTA YA MAJI

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Kundo Andrea Mathew, amefanya ziara ya kikazi Mkoani Iringa na kushiriki kikao cha pamoja na Menejimenti za IRUWASA, RUWASA, Bodi ya Maji Bonde la Rufiji, pamoja na Maabara ya Maji ya Mkoa wa Iringa. Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa mikutano wa IRUWASA na kimelenga kujadili hali ya utoaji wa huduma za maji pamoja na mikakati ya kuboresha sekta hiyo.

Akiwa katika kikao hicho, Mhe. Naibu Waziri amepokea taarifa ya hali halisi ya huduma ya maji kwa Mkoa wa Iringa, ambayo imejumuisha pia taarifa ya utekelezaji wa ufungaji wa mita za malipo kabla (Prepaid Meters). Taarifa hiyo imeonesha hatua mbalimbali zinazochukuliwa na mamlaka hizo katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, za uhakika na endelevu.

Katika hotuba yake, Mhe. Kundo amesisitiza umuhimu wa uwajibikaji, uadilifu na ubunifu kwa viongozi na watumishi wa sekta ya maji, akibainisha kuwa bila kufanya kazi kwa weledi na fikra za ubunifu, juhudi za Serikali kuboresha huduma ya maji hazitafikia malengo yaliyowekwa.

Aidha, amezitaka mamlaka zote zinazohusika na huduma za maji kufanya kazi kwa ushirikiano, kuongeza kasi ya kutatua changamoto zilizopo, na kuhakikisha miradi ya maji inayotekelezwa inaleta matokeo chanya kwa wananchi.


Posted On: 10th December, 2025
News Source: NLUPC Reporters